KITAIFA

MASTAA 14 WAMPASUA KICHWA GAMONDI

LIGI Kuu Bara imesimama kwa wiki mbili kupisha kalenda ya Fifa kwa mechi za kimataifa za timu za taifa, huku kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi kwa sasa akifunga na kuomba ili mastaa 14 wa timu hiyo walioitwa warudi salama ili kuendeleza moto kutetea ubingwa inayoushikili kwa msimu wa tatu mfululizo.

Mechi za timu za taifa zikimalizika na ligi kurejea, Yanga yenyewe itakuwa na kibarua cha michuano ya CAF ikitakiwa kuvaana na CBE SA ya Ethiopia katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kitu ambacho Gamondi ameanza kupiga hesabu zake akisaka tiketi ya makundi ya mara ya pili mfululizo.

Kikosi hicho kilianza msimu kwa kubeba Ngao ya Jamii kwa kuzishinda Simba 1-0 na Azam 4-1 kisha kuing’oa Vital’O ya Burundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 10-0 katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuifumua Kagera Sugar mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Maxi Nzengeli na Clement Mzize kabla ya ligi kusimama huku mastaa 14 wa timu hiyo kuitwa timu tofauti za taifa na kumfanya Gamondi kuwa na presha akihofia wasije wakapata majeraha na kumtibulia hesabu zake dhidi ya CBE iliyoing’oa SC Villa ya Uganda.

Gamondi alisema kwa sasa anakosa nguvu ya kujipanga sawa sawa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani analazimika kwanza kuomba Mungu wachezaji 14 waliokwenda kujiunga na timu za mataifa saba tofauti kwa ajili ya mechi za kuwania Afcon 2025 warudi salama na kwa wakati.

Mastaa wa Yanga walioitwa timu za taifa ni Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Clement Mzize, Nickson Kibabage, Mudathir Yahya, Aboutwalib Mshery  wote wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Clatous Chama na Kennedy Musonda (Zambia), Prince Dube (Zimbabwe), Khalid Aucho (Uganda), Stephane Aziz Ki (Burkina Faso), Duke Abuya ( Kenya) na Djigui Diarra (Mali).

Cha kushangaza ni kwamba washambuliaji wake watatu Dube, Musonda na Mzize wote wameitwa, hivyo kumfanya asaliwe na Jean Baleke ambaye hataweza kumtumia katika mechi ya CBE.

 

“Nimepanga kila siku kuhakikisha napata taarifa za wachezaji wanapomaliza mazoezi au mechi zao ili kujua wanajipangaje na mchezo dhidi ya CBE ya Ethiopia. Kundi hilo la wachezaji ambalo halipo asilimia kubwa ndio kikosi changu cha kwanza kilipo lakini kwa wachezaji ambao wamebaki nitakuwa na mpango maalum,” alisema Gamondi na kuongeza;

 

“Nafanya hii kwa sababu ya kuwaweka tayari ili lolote likitokea wawe kwenye eneo salama la kufanya maamuzi. Bahati mbaya mchezo wao wa kwanza unafanyika ugenini lakini kitu kinachomshusha pumzi ni kwamba Ethiopia ni kama makutano, kwani hapo kuna kituo kizuri Cha usafiri kitakachoweza kuwaungaisha wachezaji hao kutoka Mataifa mbalimbali.”

 

Akizungumza wapinzano wao, alisema kama kocha tayari amaeshaanza kusoma mbinu zao na namna walivyocheza mechi yao ya mwisho.

 

“Tayari nimeshaanza kupata taarifa za wapinzani wetu ikiwemo mikanda ya video ya mechi ya kwanza dhidi ya Villa ya Uganda hivyo tunajipanga.”

 

Wachezaji kutoka katika kikosi cha Yanga waliyoitwa katika mechi ya kufuzu Afcon 2025 jumla ni 14 wakichezea mataifa saba tofauti.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button