BAADA ya kuaminiwa kulilinda lango la Simba kwa dakika 45 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal, Aishi Salum Manula alikuwa na kiwango kizuri sana kwa kuchomoa michomo ya hatari zaidi ya mara moja.
Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa, ulimaliza kwa sare ya 1-1, goli la Simba likifungwa na Leonel Ateba, Simba ilicheza vizuri kabla ya kipindi cha pili mambo kuwa magumu kwao na hii ni kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa timu hiyo Fadlu Davids.
Mchambuzi wa soka nchini Farhan Kihamu ametoa sifa kwa nyanda hilo, ambalo lilikuwa nje kwa muda mrefu hali iliyopelekea mashabiki wengi kuwa na wasiwasi na kiwango chake.
“HOMEBOY SINA SHAKA KABISA TANGU SIKU YA KWANZA, huwa nasema kila siku Bongo hapa vipaji vingi vinakufa kwasababu watu wamekinai tu, wamechoka kuona ubora wako, wanahitaji tu kumwona Mtu mwingine, kiasili Binadamu yoyote anachukia MWENDELEZO wa ubora.”
“Simulizi yako ni kama ya Juma Kaseja Juma, watu walichoka tu ila Juma aliendelea kuonesha akaitwa Taifa Stars akitokea KMC na akaenda kulibeba Taifa kule Nairobi, HOMEBOY endelea kuonesha, uwezo upo tena mkubwa tu ila watu wamekinai, wanachukia ubora tu wakati mwingine.”
“Ukweli ni kuwa Viongozi wa Simba kutotaka kukuruhusu uondoke ni kwamba wanatambua uwezo wako, wanatambua nini kipo kwenye gloves zako, ASANTE kwa kutokata tamaa HOMEBOY tulipotoka ni mbali sana na wengi wanakutazama kama mfano, kama Kiigizi chao na ushindi wako ni ushindi wa wengi MTUA.”
“Kutoka Bonde la Mto Luhombero huko Ulanga mpaka Bonde la Mto Kilombero hapo Mkamba, wanaheshimu mikono yako na kutambua Kipaji chako, ukiona umechoka kushinda kwa ajili yako basi vaa jezi kashinde kwa ajili ya maelfu ya Watu ambao tupo proud kukuita HOMEBOY RESPECT HOMEBOY Aish Manula”