MARA Baada tu ya kutambulishwa, straika, Christian Leonel Ateba, kutoka USM Alger ya Algeria, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kushuhudia ubora wake wakati wakiivaa Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Ateba ambaye amekamilisha kikosi cha Simba baada ya dirisha la usajili kufungwa rasmi hapo juzi usiku aliliambia gazeti hili kuwa, mashabiki wa timu hiyo hawataondoka na majonzi.
Ateba alisema yeye ni mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, na amekuja katika timu ya Simba kufanya kazi aliyotumwa.
“Jina langu ni Ateba, mimi ni mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, ni mchezaji mpya wa Simba, tutaonana katika mechi dhidi ya Tabora United, nawaomba wanachama na mashabiki wote waje uwanjani kuangalia nini tunafanya, nitakuwepo katika mechi hiyo na hawataondoka kwa majonzi, badala yake watafurahi,” alitamba straika huyo.
Ateba ambaye ana umri wa miaka 25 ametua kwa Wekundu wa Msimbazi baada ya mabosi kufuata pendekezo la Kocha Mkuu, Fadlu Davids, aliyeweka wazi anahitaji kupata mshambuliaji mwingine ili kuongeza nguvu katika kikosi chake baada ya kuonekana kutoridhishwa na nyota waliopo.
Straika huyo amewahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwamo PWD Bamenda, Dynamo Douala za Cameroon na USM Alger pamoja na kikosi cha Timu ya Taifa ya Cameroon maarufu Indomitable Lions.