Makocha wa Yanga na Simba wameelezea ugumu wa mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii kati ya timu hizo Agosti 8 wakitahadharisha kwamba klabu zao zitacheza kwa makini ili kupata ushindi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na Fadlu Davids wa Simba wameeleza hayo Dar es Salaam leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo.
Kocha Gamondi amesema hakuna mnyonge katika mechi hiyo na anajua mpinzani wao ana timu mpya hivyo kwa pamoja watachukua fursa hiyo kuonesha ubora wao.
“Kimsingi mchezo huu mizani ipo sawa kwa pande zote 50/50, ni muhimu sana kuendea mchezo huu kwa umakini mkubwa,” amesema Gamondi.
Naye kocha Davids amesema ana uzoefu wa michezo mikubwa kama huo na lengo ni ushindi.
“Tunaichukua mechi hii kama mechi nyingine unahitaji kushinda ili kuanza vizuri msimu kwa kulitetea taji hili, nina uzoefu wa michezo hii mikubwa ya dabi, ukiangalia timu yetu ni mpya tutakuja na mbinu tofauti kuhakisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Davids.
Mchezo huo wa “dabi” ya Kariakoo utatanguliwa na mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Azam na Coastal Union kwenye uwanja wa New Amani, Zanzibar.