MANULA KUIPELEKA SIMBA MAHAKAMANI…JEMEDARI AELEZA KINAGA UBAGA
BAADA ya Simba kutotoa ufafanuzi kuhusu uwepo wa Aishi Manula kwenye kikosi msimu wa 2024/25 Meneja wa mchezaji huyo Jemedari Said ameweka wazi kuwa wanasikitishwa na kitendo cha Simba hivyo watachukua hatua kuona mchezaji huyo anapata haki.
Kwenye ukurasa wa Instagram ameandika namna hii: “Tunazungumza na wanasheria wetu kuona namna watakavyoshughulia suala la klabu ya Simba na mchezaji wetu AISHI MANULA kwa kitendo cha Simba KUMZUIA mchezaji kucheza soka ambacho kinapingana na kanuni za FIFA.
“Mchezaji haumwi wala hana jeraha lolote, hajawahi kupewa taarifa yoyote na klabu yake ambayo ana mkataba nayo kwa mwaka 1, kuhusiana na chochote cha klabu.
“Hajawahi kuambiwa kupima afya kwahiyo hajapima afya kama wengine, hajashirikishwa kwa namna yoyote kwenye mazoezi ya Misri mpaka timu imerudi hajaambiwa lolote na leo Simba imetangaza kikosi chake yeye hajatajwa popote mpaka Meneja wake alipolalamika ndiyo jina lake likatajwa.
“Alipata timu ambayo iliandika barua kumuomba mchezaji lakini Simba wamekataa, wao hawamtaki na kumuacha aondoke akacheze hawataki pia, mchezaji maisha yake ni mpira na Simba wanamzuia mchezaji kucheza mpira, wanasheria watatuambia kanuni za FIFA zinasemaje na zile za TFF, zinaruhusu uhuni wa namna hii?
“Mwisho Simba kama klabu inatoa meseji gani kwa wachezaji wengine? HAIKUBALIKI..!!” Aliandika Jemedari Said- Meneja wa Aish Manula.