Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmedy Ally amethibitisha kuwa Mshambuliaji wao Kibu Denis amerejea kikosini na amepata nafasi ya kuzungumza na kumalizana na Kocha Mkuu wa sasa Fadlu Davids, hivyo mambo yapo sawa.
Ahmedy Ameongeza kuwa Simba itamchukulia hatua za kinidhamu Kibu ili asirudie na iwe funzo wachezaji wengine kwawengine.
“Kibu Denis amerejea Dar es Salaam (Akitokea Norway) atakuwepo Simba Day, klabu imemsamehe ila lazima impe ADHABU kutokana na utovu wa nidhamu,” amesema Ahmed Ally.
Wakati Kibu Denis ametorokea Norway alipoitwa kufanya majaribio na timu ya Ubelgiji, Ahmed Ally alifunguka jinsi usajili wa mchezaji huyo, alivyoisumbua klabu katika kumuongeza mkataba.
“Hakuna usajili uliotutesa Simba kama wa kumuongezea mkataba Kibu Denis. Alikuwa anasema ntaongeza mkataba, ntaongeza mkataba Anapitia huku anatokea huku. Wavimba macho nao walikuwa wanamvizia Hatukulala wiki mbili.
“Watu wanasema ana goli moja. Ndio ana goli moja lakini anajituma sana. Kibu ni aina ya wachezaji ambao wanacheza kama timu za baba zao, Hakuna timu inatamani kukutana na Kibu na kukutana na balaa lake,” amesema Ahmed Ally.