CLATOUS CHAMA ATOA ONYO HILI KALI KWA SIMBA
MWAMBA wa Lusaka Clatous Chama, amefurahishwa na timu yake mpya (Yanga) kutwaa Kombe la Toyota na kuvaa medali ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kujiunga nayo akitokea Simba, huku akisisitiza kuwa yeye na wachezaji wenzake wanataka kuchukua kila kombe na taji lililo mbele yao, kwani ni muhimu sana kwa mashabiki wao.
Akizungumza juzi nchini Afrika Kusini, baada ya kutamatika kwa mchezo maalumu ulioandaliwa na Klabu ya Kaizer Chiefs, Chama alisema kombe walilopata limezidi kuwapa morali ya kwenda kutwaa taji lingine lililopo mbele yao.
Agosti 8, mwaka huu, Yanga itacheza mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao ndiyo wenye taji hilo, mchezo ukitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Nawaahidi Kilele cha Wiki ya Mwananchi watafurahi sana, waje kwa wingi uwanjani,” alisema Chama ambaye amejiunga na klabu hiyo hivi karibuni akitokea Simba na katika mechi hiyo aliingia akitokea benchini kuchukua nafasi ya Aziz Ki.
Kwa upande wa beki wa kati, Dickson Job, alisema kikosi chao msimu huu kimeongeza baadhi ya wachezaji ambao wana uwezo mkubwa, hivyo wana kikosi kipana na bora kuliko msimu uliopita, akitabiri kuwa huenda kitakuwa bora na mafanikio zaidi kuliko hapo nyuma.
“Naamini kwa mechi hizi tatu tumeshaanza kupata muunganiko kati yetu na wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu. Naamini msimu ujao tutafanya vizuri zaidi kwa sababu kuna kikosi kipana chenye wachezaji bora ukilinganisha hata na msimu uliopita,” alisema.
Yanga imemaliza mechi zake tatu maalum nchini Afrika Kusini, ikishinda mbili na kupoteza moja, ambapo ilichapwa mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani, mchezo uliochezwa Julai 21, kabla ya kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili dhidi ya wenyeji TS Galaxy, Jumatano iliyopita.