KITAIFA

MASTAA WALIOONDOKA NA WAKARUDI BONGO, SIMBA NA YANGA ZIKAWABEBA TENA

UTAMU wa Ligi kuu ya NBC unazidi kuongeza na sasa ni miongoni mwa Ligi 6 bora za Afrika, hali hii inawafanya wachezaji wengi kukimbilia kucheza Tanzania. Soka la Bongo tumekuletea majina ya mastaa kibao ambao waliondoka Bongo na baadae kurudi tena kukiwasha kutokana na utamu wa Ligi hii.

BOBAN BOREGE ZIRINTUSA

Katika orodha ya wageni walioondoka Bara kisha kurudi, huyu anaweza kuwa kiranja wao, kwani alikuja nchini na kuichezea Mtibwa, kisha akaondoka na kuzurura timu kadhaa tofauti na miaka 14 baadaye akarudi tena kuendeleza moto, japo kwa sasa anacheza Ligi ya Championship.

Ni mshambuliaji kutoka Uganda na alitamba na Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza mwaka 2009 aliyoichezea hadi 2012 alipotimkia Highfield United na baadae Dynamos FC zote za Zimbabwe.

Mwaka 2016 alitua Polokwane City ya Afrika Kusini aliyokaa nayo hadi 2018 alipokwenda Buildcon ya Zambia, pia akapita Ethiopia Bunna, Busonga United ya Uganda, kabla ya Februari 2023 kurudi tena Mtibwa kupitia dirisha dogo la msimu huo wa 2022-2023 na ulipomalizika akaenda zake Express ya Uganda.

Msimu uliopita mwamba huyo wa kucheka na nyavu aliichezea Biashara United iliyopo Ligi ya Championship na kuifungia mabao 21 kama aliyomaliza nayo Edger Williams wa KenGold.

EMMANUEL OKWI

Raia mwingine wa Uganda aliyewahi kuweka heshima kubwa Ligi Kuu. Ndiye aliyekuwa kinara wa kuja na kuondoka Bongo.

Kipindi Okwi ambacho amecheza soka la kulipwa hapa, ametwaa mataji manne ya Ligi Kuu akiwa na Simba na kuvaa medali ya ushindi ya Kombe la Mapinduzi.

Aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa mechi ya Nani Mtani Jembe msimu wa 2014/2015 na msimu wa 2018/2019 alitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na klabu hiyo.

Mara ya kwanza Okwi kuja nchini ni mwaka 2009 alipotua Simba akitokea SC Villa ya kwao Uganda na kuitumikia hadi 2013 kitwaa nao mataji mawili ya Ligi Kuu Bara 2009-2010 na 2011-2012.

Kisha alisepa zake Etoile du Sahel ya Tunisia kabla ya kuibukia Yanga ndani ya muda mfupi na baadaye kurejea Simba hadi 2015 alipouzwa Sonderjske ya Denmark, lakini alikaa nao hadi 2017 alirudi SC Villa na kurejea tena Ligi Kuu Bara kukipiga Simba hadi 2019 na alitwaa nao tena mataji mawili ya 2017-2018 na 2018-2019 kabla ya kuuzwa Al Ittihad ya Misri kisha kupita Kiyovu Sports ya Rwanda na mwaka jana kurejea Misri kukipiga Al Zarwaan SC na Erbil aliyomalizana nao mkataba na kwa sasa hana timu.

PASCAL WAWA

Wawa alijiunga na Azam FC msimu wa 2014/15 akitokea Al-Merrikh SC na aliitumikia kwa misimu miwili na baadae kurudi timu yake ya zamani na msimu 2018/19 alijiunga na Simba ambayo aliichezea misimu mitatu kwa mafanikio na baadae akatimkia Singida Fountaine Gate.

Ni miongoni mwa mabeki walioisaidia Azam FC kutwaa taji la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2015, timu hiyo ikicheza bila kuruhusu bao lolote, kisha aliondoka zake kurudi Al Merrikh ya Sudan kabla ya mwaka 2017 kurudi nchini na kujiunga na Simba aliyoichezea hadi mwaka 2022 akitwaa nao mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mbali na Ngao za Jamii na Kombe la Mapinduzi.

Pia alikuwa mmoja wa wachezaji walioisaidia Simba kurejea kwa kishindo katika michuano ya kimataifa 2018-2019 kwa kutinga makundi ikiwa ni tangu ilipofanya hivyo mwaka 2003 na kwenda robo fainali mara tatu hadi alipoondoka kutua na Singida ambayo ilimtema msimu uliopita.

HERITIER MAKAMBO

Sio jina geni kwenye soka la Tanzania kutokana na kucheza kwa misimu tofauti na 2018-2019 ndiyo ulikuwa msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara akijiunga na Yanga na kuitumikia kwa msimu mmoja tu ambao alitupia kambani mabao 17, kabla ya kujiunga AC Horoya ya Guinea.

Mkongoman huyo aliondoka akiwa ameifungia Yanga mabao 17 akisaidia timu yake kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba, lakini akimaliza nafasi ya tatu ya orodha ya wafungaji wa msimu huo nyuma ya kinara Meddie Kagere akiwa Simba aliyefunga 23 na Salim Aiyee aliyekuwa Mwadui aliyetupia 18.

Msimu wa 2021/22 mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kipenzi cha wanayanga alirudi tena nchini timu hiyo ikiwa chini ya Nasreddine Nabi, lakini mambo yake hayakuwa mazuri na aliitumikia kwa msimu mmoja na kutimkia zake Al Murooj SC ya Libya na sasa anatajwa kutua Tabora United inayocheza Ligi Kuu Bara.

CLATOUS CHAMA

Alitua Tanzania na kujiunga na Simba msimu wa 2018/19 akitokea Lusaka Dynamos FC na alicheza misimu miwili kwa mafanikio na kujiuza RS Berkane na huko hakuchukua muda mrefu kutokana na kukosa namba ya kucheza mara kwa mara na kuamua kurudi tena Simba.

Chama msimu wa 2020/21 alikuwa kwenye kikosi bora cha msimu na alitwaa tuzo ya kiungo bora, ikumbukwe pia kwa msimu wa 2019/20 alitwaa tuzo ya kiungo bora pamoja na mchezaji bora wa msimu na kwa msimu uliopita ipo mikononi mwa nahodha wa Simba John Bocco.

Alisepa Bongo na kuibukia Morocco na kwa sasa atakipiga Jangwani baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea kwa watani zao Simba baada ya kumaliza mkataba wake.

AMISSI TAMBWE

Alikuja nchini mwaka 2013 kujiunga na Simba na baada ya kuichezea kwa msimu mmoja, alitimka zake na kujiunga na Yanga aliyoitumikia misimu mitatu miwili na kuachana naye.

Katika muda wote aliocheza Tanzania, ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu zote akiwa na Yanga kuanzia msimu wa 2014/2015 hadi msimu wa 2016/2017 huku pia akitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili akiwa na Yanga.

Pia amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili tofauti ambazo ni msimu wa 2013/2014 na 2015/2016 na katika kipindi chote alichocheza Tanzania amefunga mabao 74 katika mashindano mbalimbali.

Baada ya kumalizana na Yanga alitimkia Djibut na hakuchukua muda mrefu akitumika kwa miezi sina na kuamua kurejea Tanzania akijiunga na DTB ambayo ilikuwa inashiriki Championship akaipambania na kuipandisha daraja ligi kuu na kuitwa Ihefu FC baada ya kupandisha aliachwa na kutimka tena Tanzania. Akiwa DTB aliibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 14.

OBREY CHIRWA

Ni mzoefu kwenye soka la Tanzania baada ya kucheza kwa mafanikio akiwa Yanga na baadaye kurudi tena kukipiga Azam na alicheza misimu miwili haikuwa na mafanikio kama ilivyokuwa msimu wake wa kwanza Tanzania.

Alianza kucheza Yanga akijiunga na timu hiyo kutoka FC Platinum 2016 akiitumikia timu hiyo kwa misimu miwili baadae akatimkia Nogoom FC na kurudi tena Tanzania akijiunga na Azam FC ambayo ameitumikia kwa misimu mitatu, akatua Namungo, Ihefu FC na msimu ulioisha amemalizia Kagera Sugar.

HARUNA NIYONZIMA

Alijiunga na Yanga mwaka 2011 akitokea APR ya Rwanda na akaitumikia kwa miaka sita kabla ya kujiunga na Simba mwaka 2017 alipoachana nayo na kurejea kwao Rwanda kisha akajiunga tena na Yanga dirisha dogo Januari, mwaka juzi.

Katika kipindi cha miaka tisa aliyocheza nchini, Haruna ameshinda mataji sita ya Ligi Kuu Bara nqa mara nne ametwaa akiwa Yanga na mara mbili akiwa na Simba.

Pia ana medali moja ya ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) alilotwaa akiwa na Yanga mwaka 2012, pia amecheza hatua ya makundi ya klabu Afrika mara mbili tofauti akiwa na Yanga na Simba.

Mwaka 2016 alicheza hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Yanga na msimu wa 2018/2019 alitinga hatua ya robo fainali akiwa Simba.

LUIS MIQUISSONE

Miquissone anakumbukwa kwa mengi makubwa aliyoyafanya pindi alipokuwa mitaa ya Msimbazi kuanzia Januari 2020 hadi Agosti 2021 alipotimkia Al Ahly na alishindwa kufanya vizuri.

Licha ya kuonyesha ubora Ligi Kuu Bara alishindwa kuonyesha makali hayo Al Ahly ambao waliamua kumtoa kwa mkopo Abha ya Saudi Arabia na baadae msimu huu wa 2023-2024 aliamua kurudi tena Simba na amecheza msimu mmoja tu na kuachwa na timu hiyo kutokana na kushindwa kuonyesha makali yake.

PAPY TSHISHIMBI

Alionwa na Yanga akiwa na timu yake ya Mbabane Swallow ilipokuja kucheza na Azam FC michuano ya kimataifa akaungana na wanajangwani 2018/19 akiitumikia Yanga kwa misimu miwili hadi 2020 baadae akatimkia kwao Congo akijiunga na As Vita ambayo alihudumu naho yadi 2022.

Msimu huo wa 2022 aliamua kurudi Tanzania na kujiunga na Ihefu FC ambayo hakuitumikia kwa muda na kuamua kujiunga na Tabora United ikiwa daraja la chini na kuipandisha Ligi Kuu kabla ya kuachana nayo.

AUGUSTINE OKRAH

Alitua Simba 2022 akitokea Bechem United akaitumikia kwa msimu mmoja, rekodi nzuri aliyoandika ni kuifunga Yanga akiwa na timu hiyo.

Akarudi nchini kwao na kujiunga na Bechem United na akiwa na timu hiyo alifanya vyema kwenye Ligi Kuu ya Ghana hadi kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba na katika mechi 16 ametupia mabao tisa.

Dirisha dogo la usajili msimu ulioisha Yanga walifanya mchakato wa kunasa saini ya winga huyo ambaye amehudumu kwa miezi sita tu na timu hiyo kuachana naye dirisha hili na usajili.

JEAN BALEKE

Mshambuliaji huyo Mkongomani amecheza Simba kwa msimu mmoja baada ya kusajiliwa mwa mkopo katika dirisha dogo la usajili akitokea TP Mazembe.

Amemalizana na timu hiyo na kutimkia Al Ittihad ya Libya kwa mkopo wa mwaka mmoja, aliondoka Simba akiwa ameifungia mabao sita msimu ulioisha na anatajwa kutua Jangwani msimu ujao na atavaa jezi za njano na kijani.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button