MWAMBA Aziz Ki ni mtambo wa kuvunja rekodi ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na kasi yake kuwa kwenye mwendelezo bora wakati wote kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Ikumbukwe kwamba aliibuka Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast msimu wa 2022/23 ambapo alikuwa akitajwa pia kuwaniwa na Simba inayonolewa na Juma Mgunda.
Ki aliyetambulishwa usiku wa manane ametimiza majukumu yake mchana kweupe huku akiwa na tuzo ya ufungaji bora msimu wa 2023/24 akiwa kafunga jumla ya mabao 21.
Nyota huyo kavunja rekodi zake zote ambazo aliziandika msimu wa 2022/23 ambapo kwenye upande wa kufunga alifunga mabao 9 na yote alitumia mguu wa kushoto.
Msimu wa 2023/24 Aziz kavunja rekodi ya mabao akifunga mabao 21 na katika hayo kafunga kwa mguu wa kushoto mabao 17, mguu wa kulia mabao matatu na kwa pigo la kichwa bao moja ilikuwa dhidi ya Tabora United mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Rekodi nyingine ambayo kavunja ni kufunga hat trick mbele ya Azam FC ambayo msimu uliopita hakuiandika na kawatungua makipa wawili wa Simba, mzunguko wa kwanza Aishi Manula na mzunguko wa pili Ayoub Lakred.
Hivyo makipa wote wa Simba ambao herufi zao za majina zinaanzia na A kama jina lake kawapa tabu kwa kuwatungua kwenye Kariakoo Dabi akiwa anatajwa kuwa kwenye mazungumzo na timu hiyo kuboresha mkataba wake.