UJIO WA SIMBA MPYA, WANASIMBA MJIANDAE KWA KICHEKO
BAADA ya Simba kugotea nafasi ya tatu msimu wa 2023/24 na pointi zake 69 kibindoni benchi la ufundi limebainisha kuwa kuna maboresho makubwa yanakuja hivyo timu mpya inasukwa kwa ajili ya kurejea kwenye ushindani.
Ikumbukwe kwamba ni Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba alibeba mikoba ya Abdelhak Benchikha aliyebwaga manyanga huku mchezo wake wa mwisho kukaa benchi alishuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 2-1 Simba.
Mgunda amekaa benchi kwenye mechi tisa akiambulia ushindi kwenye mechi 7 na sare mbili zote ilikuwa ugenini, Namungo 2-2 Simba ulikuwa mchezo wa kwanza kuongoza akishuhudia Willy Onana akifunga bao la uongozi na Kagera Sugar 1-1 Simba ilikuwa sare yake ya pili, Uwanja wa Kaitaba.
Funga kazi ilikuwa ni Mei 28 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 2-0 JKT Tanzania huku mwamba Onana akifunga bao la pili kwenye mchezo huo ikiwa ni funga kazi mazima 2023/24.
Mgunda amesema: “Nimeongoza timu kwenye mechi 9 kuna masuala ya kiufundi ambayo yatafanyika hasa maboresho kwa wakati ujao. Tunatambua kwamba ili timu ifanye vizuri lazima kuwe na maboresho hivyo Simba mpya inakuja.
“Huwezi kukwepa kuhusu maingizo mapya kwenye timu hilo lipo. Mashabiki watulie wawe na subira kwa kuwa kila timu ilikuwa na malengo yao mwisho kila kitu kimekuwa kama ambavyo kimetokea, tulikuwa tunapenda kumaliza nafasi ya pili lakini tumekwama ni sehemu ya matokeo.”