MALALE Hamsini, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania amesema kuwa ushindi kwenye mchezo wa kwanza wa play off dhidi ya Tabora United ni matokeo ya wachezaji kufanyia kazi makosa yaliyopita.
Timu hiyo inapambana kujinusuru kubaki ndani ya ligi ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ukisoma Tabora United 0-4 JKT Tanzania.
Kwenye mchezo ni Said Ndemla alianza kufunga bao dakika ya 9, Ismal Aziz dakika ya 20, Matheo Anthon dakika ya 81 na kamba ya nne ilifungwa na Hassan Dilunga dakika ya 90+2.
Mchezo wa pili utaamua mshindi atakayebaki ndani ya ligi ambapo mmoja atakayeshindwa atacheza na Biashara United ambayo inasubiri timu itakayopoteza ili kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara.
Malale amesema; “Tunafurahi kupata ushindi kwenye mchezo wetu jambo kubwa ni kuona kwamba tunaendelea kuwa kwenye mwendelezo mzuri kwa kuwa ushindani ni mkubwa.
“Pongezi kwa wachezaji kwa kuwa wamefanya kazi kubwa kutafuta matokeo, mechi ambazo zilipita tulikuwa tunacheza vizuri lakini nafasi tulikuwa tunashindwa kuzitumia.”