Mei 12, mwaka huu bondia wa ngumi za kulipwa nchini na mpiga debe wa zamani wa Kituo cha Mabasi Msamvu mjini Morogoro, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ atakuwa akimaliza adhabu yake. Mandonga atamaliza adhabu hiyo iliyotokana na kusimamishwa kupanda ulingoni na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kufuatia kupokea kipigo cha TKO ya raundi sita dhidi ya bondia mkongwe, Mada Maugo mwezi uliopita mjini Morogoro.
Bondia huyo ameanza kwa kufichua mambo ambayo yalimfanya kuwa kimya kwa muda mrefu kabla ya kupanda ulingoni mwezi uliopita katika pambano alilopoteza. Katika mahojiano hayo amefunguka mambo mengi na mipango iliyopo mbele yake, lakini akigusia pia maisha ya zamani ya kula mlo wa buku na sasa akiwa na uwezo wa kuingia hotelini na kuagiza chakula cha Sh15,000 nakalipa bila wasiwasi.
Hata hivyo, Mandonga anataka pambano azichape ulingoni na msanii wa muziki, Harmonize kwa sababu ametangaza vita kwenye mchezo wa ngumi huku akisisitiza yupo tayari muda wowote na milango yake iko wazi.