HATMA YA SAIDO NTIBANZOKIZA KUBAKI SIMBA HII HAPA
IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Mualgeria Abdelhak Benchikha ndiye aliyenusuru panga la kiungo wake mshambuliaji, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ kuendelea kubakia Msimbazi.
Awali kiungo huyo alikuwepo katika mipango ya kuachwa katika usajili huu wa dirisha uliofungwa jana saa 5:59 usiku, baada ya kuwepo mvutano wa kimaslahi ya mkataba.
Kiungo huyo aligomea kusaini mkataba wa mwaka mmoja aliowekewa mezani na mabosi zake huku akishinikiza kupewa miwili ambao waajili waligomea na kubariki aondoke kabla ya Benchinka kumbakiza.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, Benchikha ndiye aliyewashawishi viongozi kumbakiza kiungo huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili wenye masharti.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa suala hilo la Saido liliwagawa Viongozi kabla ya kocha huyo kupendekeza aongezewe mkataba huo wa miaka akiamini, ataongeza kitu katika mashindano yaliyokuwepo mbele yao.
Aliongeza kuwa Benchikha tangu ametua nchini anafuatilia kwa karibu kiwango cha Saido ambacho kimemvutia na kupelekea kumbakisha hapo Simba, licha ya baadhi ya viongozi kupendekeza kuachana naye.
“Haikuwa kazi rahisi Saido kubakia Simba, ni baada ya kuleta mvutano mkubwa hadi kumbakisha katika usajili huu wa dirisha uliofunga jana saa sita usiku.
“Na kama siyo kocha Benchikha kuwasilisha ripoti ya usajili ambayo ilimuonyesha Saido abakie hapo, basi jina lake lingekatwa kutokana na viongozi kutomuhitaji.
“Kikubwa walikuwa wakibishana katika ukomo wa mkataba ambaye yeye aligomea mkataba wa mwaka mmoja na kutaka miwili ambayo waligomea viongozi kutokana na umri mkubwa alionao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuzungumzia hilo alisema kuwa “Hilo suala la kiufundi zaidi, lipo chini ya kocha wetu Benchikha, lakini fahamu kuwa Saido bado mchezaji wa Simba.”