KITAIFA

GUEDE AANZA MBWEMBWE YANGA, BAADA YA KUIFUNGA SIMBA

Straika wa Yanga, Joseph Guede aliyefunga bao la pili la Yanga juzi dhidi ya Simba baada ya kupokea mpira wa pasi ndefu kutokana na Khalid Aucho kisha kuukotroo kiufundi kabla ya kumlamba chenga kipa Ayoub Lakred, amesema anaamini ataendelea kufunga sana mabao kutokana na kuaminiwa na kocha Miguel Gamondi.

Guede aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha dogo kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni, alifunga bao hilo lililowawezesha vijana wa Jangwani kushinda mabao 2-1 mbele ya Mnyama, huku akifikisha mabao matatu katika Ligi Kuu Bara. Bao la kwanza la Yanga lilifungwa kwa penalti na Stephane Aziz KI, huku la Simba likiwekwa kimiani na Freddy Michael aliyetokea benchini katika kipindi cha pili.

Kabla ya kuifunga Simba, Guede, raia wa Ivory Coast, aliyewahi pia kukipiga RS Berkane ya Morocco, aliifunga Singida Fountain Gate mabao mawili katika mechi iliyopita kabla ya kukutana na Mnyama na kusema anaona neema ya kufunga zaidi kwa mechi zilizosalia kabla ya kufungwa kwa msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Guede alisema kabla ya mchezo alijiandaa na kuamini akifanikiwa kutengenezewa nafasi hata mbili basi kati ya hizo, lazima aitumie moja, kitu ambacho kilitolea katika mchezo huo wa juzi uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Nitafunga sana, naamini katika kupambana zaidi. Baada ya kupata mafanikio nimeweza kufunga katika mchezo uliopita na leo (juzi) nimefunga tena, nafikiri ni wakati sahihi kuendeleza juhudi zangu kwa nilipoishia baada ya Simba sasa ni mchezo unaofuata,” alisema

Guede aliyefunga pia mabao mawili katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) na moja la Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iking’olewa hatua ya robo fainali.

“Kila ninapofunga huwa inanipa nguvu ya kupambana na kutafuta muendelezo mzuri zaidi hivyo naamini kama nitaendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara nitafunga sana,” aliongeza Guede aliyetumika kwa dakika 90 katika Dabi ya Kariakoo juzi.

AZIZ KI HAIKUWA RAHISI Kinara wa upachikaji wa mabao, Stephane Aziz Ki baada ya kuifunga Simba bao la tatu ndani ya misimu miwili akiwa na Yanga tangu alipojiunga nayo akitokea ASEC Mimosas amekiri haikuwa rahisi kwake kutokana na ahadi aliyoiweka ambayo ilimweka kwenye presha kubwa.

Alisema alikuwa na deni la kutakiwa kucheza bila kuwaza kuwa kuna mtu aliyemuahidi atafunga kwa ajili yake hivyo alikuwa na kipindi kigumu uwanjani, lakini anamshukuru Mungu na wachezaji wenzake kwa kucheza kwa umoja. Aziz Kl alimuahidi Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kuwa angefunga kwa ajili yake.

“Haikuwa rahisi, lakini Mungu kafanya kwa wakati sahihi kuhusu kuifunga Simba pia sio kwamba ni mipango nakuwa nimeipanga hapana, huwa inatokea tu kwasababu mechi za dabi lolote linaweza kutokea na ndio imekuwa hivyo,” KI aliyefunga mkwaju wa penalti juzi dhidi ya Simba na kufikisha bao la 15 msimu huu aliyeongeza;

“Nafurahi kuwa mmoja wa wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kuwafunga Simba msimu wangu wa kwanza kabisa nilifanya hivyo na mechi ya kwanza msimu huu tuliposhinda mabao 5-1 nilifunga bao moja na leo (jana) nimefunga ni furaha kwangu kuifunga timu kubwa na pinzani kwetu.”

Aziz Ki alisema haijaisha hadi iishe bado wana mechi nyingine za kumaliza msimu hivyo kuifunga Simba wameshasahau sasa wanaangalia mchezo mwingine ulio mbele yao ili kusaka pointi nyingine za kuirahisisha kubeba ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo.

Msimu uliopita nyota huyo alimaliza msimu na mabao tisa tu, lakini kwa sasa amefunga 15 mawili pungufu na yale yaliyowapa kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa msimu uliopita kwa Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza waliomaliza na 17 kila mmoja na Yanga imesaliwa na mechi nane kwa sasa.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button