MWAMBA MUKWALA AWEKA REKODI YAKE, KAZI BADO SANA

MWAMBA Steven Mukwala ameandika rekodi yake ya kuwa nyota wa kwanza kufunga hat trick ndani ya kikosi cha Simba kwa msimu wa 2024/25 ukiwa ni msimu wake wa kwanza.
Nyota huyo anayevaa jezi namba 11 alifanya hivyo kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa Machi Mosi 2025 baada ya dakika 90 ubao ukasoma Coastal Union 0-3 Simba.
Simba mbele ya Coastal Union msimu wa 2024/25 imekomba pointi nne mchezo wa mzunguko wa kwanza walitoshana nguvu kwa ubao wa Uwanja wa KMC, kusoma Simba 2-2 Coastal Union.
Baada ya kufunga mabao matatu anafikisha mabao 8 katika Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika huku Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi 54 vinara ni Yanga wenye pointi 58.
Leonel Ateba naye ana mabao 8 kinara ndani ya kikosi cha Simba kwenye kucheka na nyavu ni Jean Ahoua mwenye mabao 10 kama namba ya jezi yake ila huyu ni kiungo mshambuliaji.
Kazi bado inaendelea kwenye ligi ambapo kituo kinachofuata kwenye mchezo ujao wa ligi ni dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Machi 8 2025, Uwanja wa Mkapa.